Zimebaki
wiki tatu kabla Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuchukua jengo la
Bilicanas lililokodiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kuendesha biashara ya ukumbi wa
starehe.
Jengo
hilo lipo eneo la Posta jijini Dar es Salaam.Awali, NHC ilikuwa imetoa
notisi ya siku 60 kwa wadaiwa sugu ambao wamepanga katika majengo yake
akiwamo Mbowe.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu,
alisema pamoja na Bilicanas, shirika linazidai taasisi za umma, binafsi
na watu binafsi jumla ya Sh. bilioni 15.
Notisi
ya siku 60 ya kuondoka Bilicanas pamoja na majengo ya wadaiwa wengine
ilishatolewa, Mchechu alisema na kwamba sasa zimesalia wiki tatu.
Alisema
baada ya muda huo kumalizika, utekelezaji wa kuondolewa katika majengo
hayo utaanza ukiambatana na uchukuaji wa hatua za kisheria.
Mchechu
alisema mbali ya Bilicanas, wadaiwa wengine ni Wizara ya Mawasiliano na
Uchukuzi inayodaiwa Sh. bilioni mbili, Benki ya Azania (Sh. milioni
161) na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda
na Kimataifa (Sh. milioni 631).
Wadaiwa
wengine walitajwa kuwa ni Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto (Sh. bilioni 1.3), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Sh. bilioni mbili), Tume ya Utumishi (Sh. milioni 109) na
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Sh. bilioni moja.
Mchechu
alisema ukusanyaji wa madeni hayo kwa nguvu ni mkakati wa shirika hilo
kukusanya fedha ili kusaidia ujenzi wa nyumba za watumishi wanaohamia
Dodoma.
Alipoulizwa
iwapo mkakati huo una uhusiano wowote na masuala ya kisiasa kutokana na
kumtaja Mbowe kuwa ni kati ya wadaiwa sugu, Mchechu alisisitiza hakuna
uhusiano wa siasa na zoezi hilo kwani wateja wote wanachukuliwa sawa.
“Mwaka huu ujenzi unaanza Dodoma," alisema Mchechu, hivyo fedha tunazodai zitatusaidia kukamilisha uwekezaji mjini humo."
“Ndiyo
maana tumetoa kwa tunaowadai notisi ya miezi miwili, vinginevyo
wataondolewa katika majengo ya shirika kama kanuni zinavyotaka.
“Hakuna uhusiano wowote kati ya shirika kukusanya fedha linazodai na watu binafsi akiwamo Mbowe, taasisi za umma na binafsi.
“Lengo ni kukusanya madeni ambayo baadhi yake yalisimama kutokana na mengine kuwa na kesi mahakamani.”
Alisema kuwa fedha hizo zitatumika kwa ujenzi wa nyumba za watumishi 300 hadi 500 mkoani Dodoma.
Alisema ujenzi huo unatarajia kuanza mara moja na utachukua miezi 12.
Kwa mujibu wa Mchechu, Sh. bilioni 60 za ujenzi wa nyumba hizo zitatokana na fedha za ndani.
Alisema
shirika hilo limenunua ekari 240 eneo la Iyumbu, ekari saba Chamwino,
nne Bahi na Chemba ekari nne pia ikiwa ni kuunga mkono azma ya Serikali
ya Awamu ya Tano kuhamia Dodoma.
Alisema fedha nyingine zitapatikana baada ya nyumba 97 za shirika hilo zilizopo Medeli mjini Dodoma kuuzwa.
Aidha,
Mchechu alisema kitendo cha Serikali kuhamia Dodoma kitatoa fursa kwa
Jiji la Dar es Salaam kujiimarisha kibiashara tofauti na ilivyo sasa
ambapo linakwamishwa na foleni kubwa za magari kutokana na shughuli
nyingi za serikali kufanyika.
“Dar
es Salaam kuna bandari, uwanja wa ndege," alisema na kuongeza: “Hivyo
suala la kiuchumi litaimarika zaidi kutokana na shughuli nyingi za
Serikali kuhamia Dodoma. Hii itasaidia uchumi wa nchi kusambaa katika
maeneo tofauti nchini.”
Uwekezaji
wa NHC jijini Dar es Salaam upo kwa asilimia 70, alisema na kwamba
ufanisi wa Jiji utaongezeka hususani katika usafiri na sekta nyingine
kiuchumi.
No comments:
Post a Comment