DITRO YOSIA,KIGOMA
WAZIRI Mkuu wa zamani aliyegombea urais kupitia Chadema na kuungwa
mkono na mwamvuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, Edward Lowassa, amesema Jeshi
la Polisi linatumika vibaya.
Kauli hiyo aliitoa jana wilayani Mbarali mkoani Mbeya, alipokuwa
akihutubia wananchi nje ya Ukumbi wa Lutheran uliokuwa ufanyike mkutano
wake wa ndani baada ya polisi kuufunga.
Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwataka
wananchi kuwa watulivu na wasifanye fujo baada ya zuio hilo la polisi.
“Wananchi endeleeni kuwa watulivu, polisi wamezuia mkutano halali,
msifanye fujo yoyote na pokeeni maelekezo kwa viongozi kwani nitarudi
tena siku nyingine, pole sana kwa adha mliyoipata.
“Niseme Jeshi la Polisi linatumika vibaya, Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kimeamua kuivunja demokrasia ya vyama vingi na sheria na 5 ya mwaka 1992
ya uanzishwaji wa vyama vingi,” alisema Lowassa.
HALI ILIVYOKUWA
Mkutano huo ulizuiwa na polisi ambao walifunga ukumbi kwa ufunguo
jana saa 5:40 asubuhi na kuwazuia kuingia ndani mamia ya wananchi na
wanachama wa Chadema Wilaya ya Mbarali waliofika kumsikiliza Lowassa.
Alipowasili katika eneo la tukio, Lowassa alijikuta akikwama kufanya
mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika hapo baada ya kukuta askari polisi
wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mbarali (OCD), L. Muhaji
ambaye aliufunga ukumbi huo kwa kufuli.
Hatua hiyo ilimfanya Lowassa kubaki ndani ya gari lake, huku viongozi
wa Chadema wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Nyasa), Frank Mwaisumbe
pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu, Hashim Issa wakimfuata OCD juu ya hatua
yake ya kufunga ukumbi huo.
Katika majadiliano hayo, OCD Muhaji aliwajibu viongozi hao kwamba
amepokea maagizo kutoka ngazi za juu ya kuzuia mkutano huo kwa sababu
walishapewa maelekezo katika vikao vyao, na hakuna haja kwa viongozi wa
kitaifa kufanya mikutano wilayani humo.
Baada ya kusubiri kwa zaidi ya dakika 10, Lowassa alilazimika kushuka ndani ya gari na kwenda walipo viongozi hao na OCD.
Alipomuuliza OCD huyo kuhusu hatua yake ya kufunga ukumbi huo, majibu yake yalikuwa kama aliyowapa viongozi wa kanda.
“Ndugu yangu (OCD) inakuwaje hali hii? IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi,
Ernest Mangu) alisema haitakiwi polisi kuingilia shughuli za mikutano ya
ndani, sasa wapigie wakubwa wako wakupe ‘confirmation’
(wakuthibitishie) ili uachie funguo za ukumbi,” alisema Lowassa wakati
akizungumza na OCD.
Pamoja na hali hiyo, OCD huyo alipopiga simu kwa viongozi wake wa
juu, haikupokewa hali iliyomlazimu Lowassa kumpigia simu Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Amos Makalla kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ili
kupata maelezo ya suala hilo, lakini pia haikupokewa.
MTANZANIA lilipomtafuta Makalla kwa njia ya simu ili kupata ufafanuzi
wa suala hilo, simu yake haikupokewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa
simu pia haukujibiwa.
AZUIWA KWENDA RUKWA
Awali jana asubuhi, Lowassa alijikuta akikwama kwenda katika mikoa ya
Rukwa na Katavi baada ya polisi kuuzuia msafara wake kwa hofu kwamba
unaweza kuingilia ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anayetembelea
mikoa hiyo.
Lowassa alianzia ziara yake mkoani Mbeya tangu Agosti 21. Juzi
alifanya vikao vya ndani katika majimbo yanayoshikiliwa na wabunge wa
chama chake mkoani Songwe, na jana asubuhi alitarajiwa kwenda Katavi na
Rukwa.
Katika Mikoa ya Rukwa na Katavi, alitarajiwa kufanya mikutano ya ndani majimbo ya Nkasi Kaskazini, Kusini na Sumbawanga.
Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Kanda ya Nyasa),
Frank Mwaisumbe, alisema kwamba polisi walimpigia simu Lowassa juzi saa
1.00 jioni akiwa Tunduma, wakimtaka aahirishe ziara yake Mkoa wa Rukwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Gorge Kyando, alipoulizwa kwa njia
ya simu, alisema waliwashauri viongozi wa Chadema wapange siku nyingine
ya ziara kwa sababu mkoa ulikuwa na ugeni mkubwa.
Na
No comments:
Post a Comment