Wednesday, 24 August 2016
Watu watano wafariki dunia kwa ajali
WATU watano wamefariki dunia papohapo na wengine wanne kujeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na gari la mizigo wilayani Same mkoani Kilimanjaro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbrod Mutafungwa, alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 10: 45 alfajiri katika eneo la Alikacheje Sekondari, Kijiji cha Makanya wilayani Same.
Alisema gari ya Toyota Noah nambari T933 DFY iliyokuwa imebeba magazeti ya MTANZANIA yanayochapishwa na Kampuni ya New Habari (2006) Limited, ilikuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda mkoani Arusha liligongana uso kwa uso na gari ya mizigo nambari T.532 DFQ Scania semi trailer na kusababisha vifo hivyo na majeruhi hao.
“Gari hilo la mizigo lililokuwa likitoka Babati kwenda mkoani Tanga na kuendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la Riziki Mandoo mkazi wa Karatu mkoani Arusha, liligongana na gari hiyo ya Noah na kusababisha vifo vya watu watano papohapo ambao wote walikuwa ni wanaume akiwamo dereva wa Noah aliyefahamika, Kiwanga Dominick (37) mkazi wa Kahe wilayani Moshi pamoja na majeruhi wane,” alisema.
Alisema miili miwili ya marehemu ndiyo iliyotambulika ikiwamo ya dereva wa gari hilo pamoja na mtu mmoja, Inocent Massawe (25), mkulima na mkazi wa Kibosho huku marehemu wengine watatu wakiwa bado hawajaweza kutambulika.
Aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Juma Kobasi (36) Simon Kaaya, Lita Ulutu (46) na Bakari Mndeme (31) na majeruhi watatu kati yao wamepelekwa kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa KCMC.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment