KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jijini
Arusha, Medest Meikoki amesema kuyumba kwa chama hicho katika Jiji la
Arusha na kusababisha upinzani kuongoza kutokana na makundi yaliyopo
ndani ya chama hicho.
Akizungumza mjini hapa jana, Meikoki
alisema aliamua kustaafu siasa baada ya kusulubiwa na makundi hayo
ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa na nguvu katika miaka ya 2000.
Alisema katika jiji hili kulikuwa na makundi mawili ya G7 na G13 ambayo yalikuwa na nguvu katika miaka hiyo.
Kada huyo, alisema bado baadhi ya wana
CCM waliojeruhiwa na makundi hayo wana hasira dhidi ya chama chao na
kuamua kukaa pembeni na kuacha wenye pesa wafanye watakavyo, lakini
waliapa chama hakitachukua jimbo hilo kamwe.
Alisema hatua za ziada zinatakiwa
kuchukuliwa na viongozi wa juu wa CCM wa kuwarudisha kundini
waliojeruhiwa na makundi hayo bila ya sababu za msingi vinginevyo,
upinzani utaendelea kuongoza.
Kada huyo aliendelea kusema kuwa makundi
ya kisiasa ya G7 na G13 ndiyo yamekivuruga chama na kuifikisha siasa ya
Arusha kuwa taabani kwani waliokuwa wakichaguliwa walikuwa ni viongozi
wasiokuwa na sifa za kuongoza chama hicho.
Alisema, kundi la G7 lilikuwa kundi
lenye uwezo mkubwa wa kifedha ambapo wafanyabiashara wakubwa wa Arusha,
walikuwa katika kundi hilo na walikuwa wakiamua wanavyotaka na
ukipingana nao unang’olewa.
Kada huyo alisema, kundi la G13 lilikuwa
kundi la wanasiasa wenye kujua siasa za Arusha na nchi kwa ujumla na
walikuwa wapambanaji lakini walikuwa ni watu wa kawaida tu wasiokuwa na
fedha, lakini wenye mikakati ya kutaka chama kishike hatamu.
Alisema yeye aliwahi kushughulikiwa
mwaka 2000 ndani ya chama na kundi la G7 kwani katika kura za maoni za
ndani ya chama, alishinda lakini kundi hilo halikuridhika na likaamua
kumtoa mwanaCCM na kumsimamisha upande wa Chama cha Tanzania Labour
(TLP) ili kupambana naye kwenye udiwani wa kata ya Darajambili.
Kada huyo alisema kundi hilo
lilifanikiwa, kwani TLP ilishinda katika kiti cha udiwani katika kata
hiyo na yeye kuanguka vibaya ingawa awali alishinda kwa kishindo katika
kura za maoni ndani ya chama
Alisema baada ya kushughulikiwa mwaka
2000 aliamua kujikita katika kushauri badala ya kugombea na alipoamua
kuingia tena kwenye siasa mwaka 2005, alishughulikiwa tena na akaamua
kustaafu na kubakia kuwa mshauri hadi sasa.
No comments:
Post a Comment