Wanafunzi wa vyuo katika jimbo la Texas, Marekani wameruhusiwa kuingia na bunduki darasani.
Hii ni baada ya maprofesa wawili
kushindwa kwenye ombi lao la kutaka mahakama izuiwe kutekelezwa kwa
sheria mpya inayowaruhusu wanafunzi kubeba bunduki bila kuzionyesha
hadharani.
Jaji katika mji wa Austin alipuuzilia
mbali madai ya wahadhiri hao kwamba kuwepo kwa bunduki huenda kukawa
hatari kubwa iwapo mjadala mkali utazuka darasani.
Mwanasheria mkuu wa Texas, Ken Paxton, ambaye ni wa chama cha Republican, aliunga mkono uamuzi wa jaji.
Alisema raia wanaotii sheria wana haki ya kujilinda hata wakiwa kwenye vyuo vikuu.
Chama cha Republican kinaamini
kutekelezwa kwa sheria hiyo kunaweza kuzuia visa vya watu kuuawa kwa
wingi na watu wenye bunduki kwa sababu wanaweza wakajilinda.
Jimbo la Texas lilipitisha sheria ya
kuwaruhusu raia kubeba bunduki bila kuzionyesha hadharani miaka 20
iliyopita ingawa watu hawakuruhusiwa kuingia nazo vyuoni.
Hilo lilibadilishwa wiki tatu zilizopita kupitia marekebisho ya sheria.
No comments:
Post a Comment